Azam FC kuvaana na Mbeya City.

By: Frank Nickson Mapunda
23 2018
0
  Share on:                 

Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, wataanza kampeni ya kusaka taji la Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) kwa kuvaana na Mbeya City kesho katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam ikiwa na historia ya kuvutia kwenye dimba lake hilo.

Kwa mujibu wa Bin Zubeiry, Azam FC itamenyana na wabishi hao wa jijini Mbeya, katika mchezo wake wa kwanza wa ligi hiyo utakaonza majira ya saa 1: 00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Matajiri hao wa viunga vya Azam Complex, wataingia dimbani wakiwa wanashikilia rekodi ya kuwa timu pekee inayoanza kampeni ya kuwania taji la ligi msimu huu ikiwa haijapoteza mchezo wowote katika mechi saba za mwisho za ligi ilizocheza nyumbani msimu uliopita.

Katika mechi hizo saba za mwisho za nyumbani, Azam FC imeshinda mara sita ikizichapa Ndanda (3-1), Singida United, Mwadui (zote 1-0), Mbao (2-1), Majimaji (2-0), Tanzania Prisons (4-1) na kutoka sare tasa moja dhidi ya Njombe.

Mara ya mwisho Azam FC kupoteza mchezo wa nyumbani kwenye ligi, ilikuwa ni miezi saba iliyopita ilipofungwa na Yanga mabao 2-1 (Januari 27, 2018), bao la Azam FC likifungwa na Shaaban Idd, aliyehamia Club Deportivo Tenerife ya Hispania.

Kwa mujibu wa takwimu, rekodi hiyo inaonyesha Azam FC inayonolewa na Mholanzi Hans Van der Pluijm akisaidiwa na kocha wa zamani wa Mbeya City, Juma Mwambusi, ni timu ngumu hasa inapotumia uwanja wake wa nyumbani kwani katika mechi 15 za ligi ilizocheza Azam Complex msimu uliopita, imeshinda mechi 11, ikipata sare tatu na kufungwa mmoja.

Hivyo rekodi hiyo inaibeba Azam FC dhidi ya Mbeya City, licha ya mechi nyingi za timu hiyo kuwa na ushindani hasa wanapocheza ndani ya dimba hilo linalomilikiwa na matajiri hao, ambao wametoka kutwaa taji la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) kwa mara ya pili mfululizo ikiifunga Simba mabao 2-1 kwenye mchezo wa fainali.

Kihistoria timu hizo zimekutana mara 10 kwenye ligi, tangu timu hiyo ya jijini Mbeya ilivyopanda daraja mwaka 2013, Azam FC ikiwa imeshinda asilimia 95 ya mechi zote ikiibuka kidedea mara tano, sare nne na kupoteza mara moja.


Maoni
Currently there are no comments for this topic!
Acha maoni yako