Afariki Dunia baada ya kushambuliwa na Kiboko

By: Frank Nickson Mapunda
23 2018
0
  Share on:                 

Mtu aliyefahamika kwa jina la Castory Mwaituro, amefariki dunia baada ya kushambuliwa na mnyama aina ya kiboko alipokuwa anavua samaki kwenye bwawa ka Mtera.

Mwaituro alikumbwa na mkasa huo Jumatatu wiki hii kwenye bwawa hilo katika kijiji cha Mnadani Mabati, kata ya Izazi wilayani Iringa.

Akizungumza na Nipashe juzi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnadani, Yared Mlula, alisema viboko hao wamekuwa wakiwadhuru wavuvi ambao wamekuwa wakifanya shughuli hiyo kwenye bwawa hilo.

Kutokana na tukio hilo, Diwani wa Izazi, Golden Mzinga, ameiomba serikali kuwavuna viboko hao ambao wamekuwa wengi, hivyo kusababisha wavuvi kushindwa kuvua samaki.

Alisema wananchi wengi katika kijiji hicho ni wavuvi ambao wanategemea vipato vyao kutokana na shughuli hiyo, hivyo kuwapo kwa viboko kwenye bwawa hilo kumekuwa kikwazo kwao.

Alisema tukio la kuuawa kwa Mwaituro ni la tatu katika kipindi kifupi. Aliwataja wengine waliouawa kuwa ni Patrick Kibehe na Sulupia Longo.

Kwa mujibu wa diwani huyo, viboko hao wanatesa wananchi wa kijiji hicho hatua ambayo inasababisha kupoteza nguvu kazi.

Naye mkazi wa kijiji hicho, Emmanuel Gama, kutoka kitongoji cha Mabatini, ambaye alikuwa na Mwaituro wakati mkasa huo ukitokea, walikuwa kwenye mtumbi wakati wakikagua nyavu na ndipo kiboko huyo alipotokea na kuwashambulia.

“Wakati tunaendelea kukagua nyavu, ghafla kiboko aliibuka na kupiga mtumbwi juu na tukaangukia kwenye maji na kuanza kuogelea. Baada ya muda tulichoka na kiboko alimfuata mwenzangu na kuzama naye majini,” alisema.

Hata hivyo, alisema hakukata tamaa kwa kuwa alimfuata rafiki yake na mtumbwi mwingine kwa lengo la kumuokoa na kumkuta akiwa katika hali mbaya. Alisema alimchukua kumpeleka hospitalini lakini alipoteza maisha wakiwa njiani.

Akizungumzia changamoto hiyo, Ofisa Wanyamapori wa Wilaya ya Iringa, Fatuma Juma, alisema wamesharipoti katika idara ya wanyamapori kuomba wawavune viboko hao ili kupunguza matukio ya watu kupoteza maisha.


Maoni
Currently there are no comments for this topic!
Acha maoni yako