Serikali yatoa maagizo mazito, yazuia mitambo ya kuchimbia madini.

By: Frank Nickson Mapunda
09 2018
0
  Share on:                 

Serikali imeiagiza Tume ya Madini Tanzania, kuzuia mali na mitambo yote ya Kampuni ya Canaco inayomiliki leseni ya Uchimbaji Madini ya dhahabu, kutokana na kukiuka masharti ya leseni hiyo.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji madini katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Pia, Waziri Biteko ameagiza kampuni hiyo iliyoko katika Kijiji cha Magambazi Wilayani Handeni Mkoani Tanga, ipewe hati ya makosa kwa sababu ya kwenda kinyume na Sheria ya Madini yam waka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 pamoja na kanuni za mwaka 2018.

Sambamba na hilo, amemuelekeza Kamishna wa Tume ya Madini Dkt.Athanas Macheyeka kumpa mwekezaji huyo hati ya makosa (default notice) kwa ajili ya kurekebisha makosa waliyonayo kwenye leseni ya uchimbaji wa madini na kama watashindwa kurekebisha makosa kwa muda uliotajwa na sheria, leseni yao ifutwe wapewe wawekezaji wengine.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi katika sakata la utoroshwaji wa Carbon zenye madini ambazo ziliibwa usiku kutoka eneo hilo na kupelekwa mkoani Mwanza kwa ajili ya kuyeyushwa ili kupata dhahabu kinyume cha utaratibu.

Waziri Biteko alisema kuwa mwekezaji huyo awali alifika katika Wizara ya Madini na kuomba kibali cha kusafirisha carbon tani 2.23 kwenda mkoani Mwanza katika kiwanda cha JEMA AFRICA LTD kwa ajili ya kuchenjuliwa lakini wakanyimwa kutokana na matatizo yao ya ndani lakini baadae wakachukua kibali cha kughushi kutoka Dodoma kwa ajili ya kusafirishia carbon kupeleka Mwanza.


Maoni
Currently there are no comments for this topic!
Acha maoni yako